Amesema mipango ya kuliongezea thamani zao la karafuu na kuyatambua mashamba ya Serikali inalenga la kuwaongezea kipato wananchi na kuwawekea utaratibu mzuri utakaowezesha kuyamiliki na kuyatumia vyema na kwa uadilifu mashamba hayo.
Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kushiriki katika shughuli za uchumaji na uchambuaji wa karafuu katika kambi ya uchumaji karafuu ya mkulima Mohammed Kai Bakari iliyopo Kifundi,Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa tafiti zitaendelea kufanywa kwa lengo la kuliongezea thamani zao la karafuu ambapo aliwataka wanasayansi kuongeze kasi katika tafiti hizo ili kuuongeza tija kwa wakulima na Serikali. Alisema kuliongezea thamani zao la karafuu ni nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo bei itaongezeka na heshima ya karafuu itaongezeka.
Alisema utaratibu wa sasa ambapo wakulima wa karafuu wanauza karafuu zao katika Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) baada ya kukaushwa na ZSTC kuuza kwenye soko la dunia, haziipi faida kubwa serikali wala mkulima kuliko ambavyo zao hilo lingeongezwa thamani.
Aidha, Dkt. Shein alisema kuwa Serikali inaendelea na utaratibu wa kuyatambua mashamba yake yote na baadae itaweka utaratibu mzuri wa kuwamilikisha wakulima wanaoweza kuyaendeleza na kuyatumia vizuri.
Alifahamisha kuwa Serikali haina nia wala lengo la kuwanyanganya wakulima mashamba ya karafuu bali ina mpango wa kuyatambua mashamba ya Serikali na heka. Alisema kuwa kila mwenye haki ya kupewa shamba au heka atapewa kwa mujibu wa utaratibu na wale wenye kuyashughulikia mashamba hayo hivi sasa watapewa kipaumbele.